here

Tuesday, August 22, 2017

Viongozi wa Serikali mbaroni kwa mauaji ya Wanawake Watano


Watu 32 wamefikishwa mahakamani kujibu shtaka  la mauaji ya wanawake watano yaliyotokea katika Kijiji cha Undomo Kata ya Uchama wilayani Nzega.

Miongoni mwa waliofikishwa mahakamani jana Jumatatu na kusomewa shtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Nzega, Sarafina Nsana wamo viongozi wa serikali ya kijiji hicho na  wengine wa ngazi ya kata.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Melito Ukongoji aliiambia mahakama kuwa Julai 25, washtakiwa kwa pamoja, wakiwa katika kijiji cha Undomo waliwashambulia kwa kuwapiga na kuwachoma moto hadi kufa wanawake watano kwa tuhuma za imani potofu za ushirikina.

Akisaidizana na mwenzake, Agustino Nshimba mwendesha mashtaka  huyo aliwataja waliouawa katika tukio hilo kuwa ni Nsuku Masali, Ester Kaswahili, Christina Saidi, Mwashi Mwinamila pamoja na Kabula Kagito.

Waliosomewa  mashtaka  ambao  hata hivyo  hawakutakiwa kujibu  lolote kwa  sababu mahakama  hiyo haina mamlaka ya  kusikiliza  na  kuamua mashauri ya  mauaji ni pamoja na Mtendaji wa Kata ya Uchama, Malewa Maroji, Diwani  wa Kata hiyo, Karoli Massanja, Kiongozi  wa  Sungusungu, Dotto Saraganda, mwenyekiti  wa kijiji, Ramadhani Kulwa na mtendaji wake, Rauliani Sanyiwa.

Washtakiwa wengine ni Dotto Saraganda (49), Taus Ngassa (40), Pill Kapewi (25), Leons Sospeter (36), Issah Eliudi (20), Nhungulu Sospeter (25), Saidi Nsabi(25), Emmanuel Pius(18), Estar Muhamila(25), Tatu Thomas (35), Thotunatus Ngelera (30), Milika Daudi (36), Kisuge Ntemi(31), Kulwa Kizinza (40), Shija Masali (35), na Kulwa shomali(31).

Wengine ni Selelo Mashandete (46),  Steven Saraganda (60), Paul Christoph (60), Makuya Athumani(42), Peter Mapalala(21), Maganga Daudi (19), Omary Seleli (20), Paul Emmanuel (51),Charles Kiberiti (26), Emmanuel Mihayo (27), Shomali Nhyama (75), pamoja na Shija Shomali (20).

Shauri hilo imeahirishwa hadi Septemba 4, itakapotajwa tena na muda wote wakati washtakiwa wakisomewa mashtaka dhidi yao,  jeshi la polisi liliimarisha ulinzi kuzunguka eneo la mahakama.

No comments:

Post a Comment