here

Monday, August 28, 2017

Kesi ya Kupinga Ushindi wa Uhuru Kenyatta Yaanza Kusikilizwa Kenya

Mahakama Kuu nchini Kenya imeanza kusikiliza kesi ya kupinga ushindi wa Rais wa Kenya,Uhuru Kenyata, iliyotakiwa kuanza kusikilizwa jana.

Kesi hiyo ilitakiwa kuanza jana   jioni baada ya kumalizika kwa hatua ya kwanza iliyofanyika juzi kwa pande zote tatu yaani upande wa NASA, Jubilee na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo(IEBC) kuwasilisha mahakamani hoja zao za maandishi.

 Msajili wa Mahakama hiyo, Esther Nyaiyaki akinukuliwa na  gazeti la Kiingereza la Standard nchini humo bila kueleza mabadiliko hayo alisema itasikilizwa leo.

Kesi hiyo inatokana na uamuzi wa Muungano wa vyama vya upinzani NASA chini ya mgombea wake Raila Odinga kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8, wakidai kuwa haukuwa wa haki na huru.

Odinga amepinga  matokeo yaliyotangazwa Agosti 11, mwaka huu na Tume hiyo yakimtambua Rais Uhuru Kenyatta wa Muungano wa Jubilee kuwa mshindi wa kiti cha urais katika ungwe ya pili akipata kura 8, 203, 290 sawa na asilimia 54.27 huku mpinzani wake mkuu, mgombea wa Muungano wa upinzani wa NASA, Raila Odinga akIpata kura milioni 6,762,224 sawa na asilimia 44.74.

Odinga hakukubaliana na matokeo hayo hadharani na aliamua kuwasilisha stakabadhi zake mahakamani hapo ikiwa ni saa nane kabla ya tarehe ya mwisho. Baadaye, Agosti 24, mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kwa upande wao, pia waliwasilisha stakabadhi zao kuhusiana na kesi hiyo.

Odinga ambaye alikuwa ni miongoni mwa wagombea nane wa kiti hicho cha urais, alilalamika pia kuwapo hujuma za Rais Uhuru Kenyatta kutumia mamlaka yake vibaya katika kuingilia mfumo wa tume hiyo

No comments:

Post a Comment