here

Thursday, August 10, 2017

Siku za Kichuya kuishi Simba zinahesabika

KLABU moja inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Misri, imewasilisha rasmi ofa ya Dola za Marekani 80,000 (Sh. milioni 177.4) kwa ajili ya kumnunua mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, imefahamika.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa viongozi wa Simba zimeeleza kuwa klabu hiyo imeridhishwa na kiwango cha Kichuya na mazungumzo ya awali yameshafanyika kuhusiana na kumnunua mshambuliaji huyo.

Chanzo chetu kimeeleza kabla ya viongozi wa Simba kufikia uamuzi wa kumuuza Kichuya, walihitaji kumwangalia mshambuliaji wao mpya kutoka Ghana, Nicholas Gyan, ambaye juzi naye alikuwa ni mmoja wa nyota waliotambulishwa na kuonyesha kiwango kilichowavutia mashabiki wa timu hiyo.

"Kichuya anaondoka wakati wowote, na Waarabu hao wanasema watampa mkataba moja kwa moja, wameridhika na kiwango chake, hawahitaji kumfanyia majaribio yoyote,” kilisema chanzo chetu.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara, alipoulizwa alisema ni mapema kuzungumzia suala la mchezaji huyo hasa baada ya dirisha la usajili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kufungwa.

Kichuya ambaye ni mchezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars), alijiunga na Simba msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani Morogoro na mkataba wake na Wekundu wa Msimbazi umebakiza mwaka mmoja.

Endapo Kichuya atafanikiwa kusajiliwa na klabu hiyo, itakuwa ni faida kwa wachezaji wa Stars wanaocheza nje ya nchi kuongezeka.

Kikosi cha Simba kinatarajia kuendelea na mazoezi yake jijini na kati ya kesho na Jumamosi kitaelekea Morogoro kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar yenye lengo la kuchangia damu.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alisema licha ya kupata ushindi katika mechi dhidi ya Rayon iliyopigwa Uwanja wa Taifa juzi, bado atawaimarisha nyota wake kwa lengo la kujiandaa kusaka ushindi kwenye mechi zote watakazocheza

No comments:

Post a Comment