here

Monday, August 21, 2017

Marekani na Korea Kusini wafanya mazoezi ya pamoja ya jeshi

Korea Kaskazini tayari imelaani mazoezi hayo ikisema kuwa hatua hiyo ni sawa na kumwaga mafuta kwenye moto.

Marekani na Korea Kusini wanafanya mazoezi ya kila mwaka ya jeshi, ambayo mara nyingi huighadhabisha Korea Kaskazini licha ya wito wa kutaka mazoezi hayo yasifanyike.

Wiki iliyopita Korea Kaskazini ilionekana kulegeza kamba baada ya kutisha kuwa itarusha makombora kwenda kisiwa cha Marekani cha Guam, lakini tena ikasema kuwa itafuatilia mienendo ya Marekani.

Korea Kaskazini tayari imelaani mazoezi hayo ikisema kuwa hatua hiyo ni sawa na kumwaga mafuta kwenye moto.

China na Urusi mwezi Julai zilipendekeza kusitishwa mazoezi ya kijeshi ili nayo Korea Kaskazini iache kuyafanyia majaribio makombora.

Marekani inasema kuwa mazoezi hayo yatawahusisha wanajeshi 17,500 wa Marekani na yatadumu kwa kipindi cha siku kumi.

Marekani na Korea Kusini hufanya mazoezi ya kijeshi mara mbili kwa mwaka yanayowashirikisha idadi kubwa ya wanajeshi na zana za kivita.

Mazoezi hayo hujumuisha ya ardhini , baharini na angani. Mazoezi hayo ambayo hufanyika Korea Kusini pia hujumuisha mafunzo jinsi ya kukabiliana na ugaidi na mashambulizi ya kemikali.

Korea Kusini hutuma wanajeshi 50,000 huku Marekani nayo ikituma kati ya wanajeshi 25,000 na 30,000.

Mazoezi hayo pia wakati mwingine hushirikisha wanajeshi kutoka nchi washirika na mwaka uliopita nchi zingine tisa zilijiunga nayo.

No comments:

Post a Comment