here

Thursday, August 10, 2017

MAFANIKIO HAYANA NJIA FUPI KAMA UNAVYODHANI

Tuelewe hakuna njia ya mkato katika maisha

Maisha ni safari moja ndefu yenye kila aina ya changamoto ambazo mwanadamu anakabiliana nazo.

Barabara ya maisha imejaa kila aina ya vikwazo ambavyo mtu anatakiwa avivuke ili kuelekea kwenye mafanikio. Kila mtu ana mbinu au njia zake za kukabiliana na changamoto hizi.

Ikumbukwe kwa kuwa tupo duniani hatuna budi kupambana na vikwazo hivi, ili kufikia malengo tuliyojipangia.

Kuna baadhi ya watu wanadhani kuwa mafaniko yanaweza hupatikana ndani ya siku mmoja. Kuna msemo mmoja maarufu uliozoeleka masikioni mwetu kuwa ‘Roma haikujengwa kwa siku moja’ .

Pia, wengine walidiriki kuja na msemo kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha. Misemo hii miwili inadhihirisha kuwa hakuna njia ya mkato katika kuyafikia mafanikio.

Hivyo, mafanikio ya kweli katika maisha ni mchakato ambao kukamilika kwake kunahitaji subira, kujituma na kujitahidi katika kazi. Watu wanatakiwa wawekeze nguvu zao katika katika kazi na wajiwekee mipango endelevu ili waweze kujiletea maendeleo.

Ukiangalia kwa makini historia za watu wengi waliofanikiwa katika maisha ndani na nje ya nchi yetu, utagundua kuwa hakuna aliyepata mafanikio bila kuvuja jasho. Bila shaka walifanya kazi kwa bidii wakiwa na malengo na hawakukata tamaa hata pale walipokwama.

Kushindwa kwao kuliwapa ari ya kujaribu tena na tena na kisha kusonga mbele mpaka wakafika pale walipo sasa. Hivyo basi, subira na kutokata tamaa ni kanuni ya msingi kabisa katika kuyaendea mafanikio.

Katika kuielewa nadharia hii kuwa maisha hayana njia ya mkato, hebu tuiangalie Ujerumani na watu wake. Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945 Ujerumani ilikuwa imeharibiwa vibaya kiasi cha kutotamanika.

Hata hivyo, iliwachukua Wajerumani si zaidi ya miaka 20 kurejea kwenye mafanikio yao. Leo hii ni nchi kubwa yenye viwanda na iliyojengeka vizuri.

Wataalamu wanasema kwamba Wajerumani si watu wenye akili sana kushinda wengine wala hawana vipawa vya ajabu kuliko watu wengine, bali sababu kuu ya kuendelea kwao ni kuwa na nidhamu na utambuzi wa wajibu ambao umekuwa ni tabia ya taifa zima.

Kila maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia waliyoyapata yanatokana na msingi huo. Utamaduni kama huo walionao Wajerumani ni aghalabu sana kuukuta katika nchi zinazoendelea hususan zile za Afrika.

Ndiyo maana wakati nchi kama Tanzania inalalamika kuwa moja ya sababu ya kudorora kwa uchumi wake ni Vita ya Kagera vya mwaka 1978, Ujerumani imepigana vita kuu mbili za dunia, yaani kutoka 1914-1918 na 1939-1945 lakini ina maendeleo makubwa yasiyo kifani.

Nchi nyingi za Kiafrika na watu wake zimekuwa na utamaduni wa kupenda kutoa visingizio ili kuhalalisha kushindwa kwao katika masuala mbalimbali. Utamaduni huu una madhara makubwa kwa mtu binafsi na taifa kwa jumla.

Watu wana njia nyingi katika kutafuta maisha mazuri. Njia hizi zipo za halali na haramu. Baadhi ya watu hawatofautishi kati ya njia za halali na haramu ili mradi tu wafanikiwe katika waliyoyakusudia.

Mtu anaweza kuua, kuiba, kufanya biashara ya dawa za kulevya na hata kujiingiza katika vitendo vya ufisadi ilimradi tu afanikiwe.

Kwa yakini, mtu yeyote mstaarabu na anayejali mustakabali mwema wa jamii, hawezi kuitafuta mali kwa njia kama hizi zenye madhara kwa jamii.

Hata hivyo, nieleweke kuwa si vibaya kuwa na ukwasi hata uliokithiri ilimradi tu njia za kuupata ni za halali na zisizo na madhara kwa mtu mmojammoja na jamii kwa jumla

No comments:

Post a Comment